Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka viongozi wa kuteuliwa kuanzia ngazi ya ukuu wa mkoa mpaka ngazi za chini, kujenga ushirikiano na uhusiano mzuri baina yao ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao, vinginevyo hatasita kuchukua hatua.
Ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es salaam wakati kikao cha wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji, katika kikao kazi kati yake na viongozi hao kilichofanyika Ikulu Jijini.
“Ni matumaini yangu baada ya kikao hiki cha leo sote tutakwenda kwa mwelekeo mzuri na zaidi, nendeni mkachape kazi mimi ndiye niliyewaweka kwenye nafasi hizo na ninawafuatilia utendaji kazi wa kila mmoja wenu,” amesema Rais Magufuli.
Hata hivyo, amewaonya baadhi ya viongozi hao ambao wamekuwa na migogoro baina yao na hivyo kuathiri utendaji kazi na amesema endapo vitendo hivyo vitaendelea hatasita kuchukua hatua ikiwa ni pamoja kuwaondoa katika nyadhifa zao.