Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limeipa onyo klabu ya Al Hilal ya Sudan kufuatia fujo zilizosababishwa na Mashabiki wa klabu hiyo, wakati wa mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya St George ya Ethiopia.

Al Hilal ilicheza nyumbani Uwanja wa Al Hilal mjini Khartoum-Sudan Jumapili (Septemba 18) dhidi ya Mabingwa hao wa Ethiopia na kuibuka na ushindi wa 1-0, ulioivusha kwa faida ya bao la ugenini baada ya kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza kwa 2-1.

Mashabiki wa klabu hiyo kongwe nchini Sudan walifanya fujo kwa kuwasha miale ya moto na kusababisha moshi uliotapakaa eneo la kuchezea, hali ambayo ‘CAF’ wametoa taarifa za onyo kuelekea mchezo wao wa pili dhidi ya Young Africans.

Hata hivyo tayari Uongozi wa klabu hiyo umekataa katakata mchezo wao dhidi ya Young Africans ya Tanzania kuoneshwa Mubashara (Live), licha ya kutengewa ofa za donge nono ili kuuza haki za matangazo ya mchezo huo.

Hii ni mara ya pili kwa Uongozi wa Al Hilal kukaa kuuza Haki za Matangazo wakifanya hivyo katika mchezo uliopita dhidi ya St George ya Ethiopia.

CAF imekua ikitoa Haki za matangazo kwa timu mwenyeji katika michezo ya Hatua ya Mtoano, huku Shirikisho hilo likijipa nafasi ya kumiliki Haki za Matangazo kuanzia Hatua ya Makundi na kuendelea.

Waziri Mchengerwa ataka ushindi Kimataifa
Simba SC yatoa tahadhari Kimataifa, Ligi Kuu