Beki wa Kulia wa Simba SC Shomari Salum Kapombe amefunguka kwa mara ya kwanza baada ya kurejea kwenye kikosi mwishoni mwa Juma lililopita, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar.

Simba SC ilikua mwenyeji katika mchezo huo uliounguruma Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiibuka na ushindi wa mabao 5-0 na kujiongezea alama kwenye msimamo Ligi Kuu.

Kapombe alionekana kwa mara ya kwanza akiitumikia Simba SC, baada ya kuwa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha ambayo yalikua sababu ya kutojumuika na wenzake kwenye michezo ya Ligi Kuu na ile ya Kimataifa msimu huu 2022/23.

Beki huyo amesema hatua ya kurejea kwake uwanjani, imekua faraja kubwa sana kwake, na hana budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuwezesha tena kuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC.

“Siku zote huwa ninamtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila nitakalolifanya, kabla ya mchezo wetu na Mtibwa Sugar nilifanya hivyo na ninamshukuru kwa kuniwezesha kumaliza salama.”

“Ninaamini dua hunisaidia kwa kunikinga na mambo mengi ninapokua katika shughuli zangu za kucheza mpira na mambo mengine, hata nilipokua na majeraha nilitanguliza yeye na ndio maana ameniwezesha kurudi tena Uwanja nikiwa na afya njema kama zamani.”

“Haikuwa rahisi kwangu kufika hapa nilipofika hadi kuonekana nikiwa na wenzangu katika kikosi cha Simba SC, Ninamshukuru sana Mungu kwa hili, ninaamini ataendelea kuniwezesha kufanya makubwa kwa kushirikiana na wenzangu ilikuifikisha Simba SC katika mafanikio tunayotarajia msimu huu.”

“Najua Mashabiki na Viongozi walikua wakiniombea ili niweze kurudi katika hali yangu ya kawaida na nianze kucheza tena soka, kwa hilo na mimi ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu awalipe kwa dua zao ambao walitumia muda wao kuniombea, sasa nipo kikosini na nitaendelea kuwepo kwauwezo wake.” amesema Kapombe

Kwa muda wote ambao Kapombe alikuwa majeruhi, nafasi yake ilizibwa na Beki Israel Patrick Mwenda ambaye alionyesha uwezo mkubwa kwa kuisaidia Simba SC kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na ile ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Kocha Nabi: Safari hii haturudii makosa
Nishati safi: Tibaijuka amshauri Makamba kukaa na wadau