Mkuu wa wapiganaji wa Wagner, Yevgeny Prigozhin ameapa kupindua uongozi wa juu wa jeshi la Urusi huku Moscow ikimshutumu Kiongozi huyo kwa kutishia vita vya wenyewe kwa wenyewe na kwamba kundi hilo linafanya uasi wa kutumia silaha.
Hatua hiyo, inafuatia Prigozhin kuchapisha ujumbe wa sauti kwenye programu ya mtandao wa kijamii wa Telegram, akidai kuwa wapiganaji wake walikuwa wamevuka kutoka Ukraine hadi mji wa mpaka wa Urusi wa Rostov-on-Don, na kwamba wangepigana na mtu yeyote ambaye atajaribu kuwazuia.
Alisema, “Sote tuko tayari kufa. Wote 25,000, na wengine 25,000,” alisema, baada ya awali kuwashutumu wakuu wa Urusi kwa kuanzisha mashambulio dhidi ya watu wake akidai kuwa si sawa kwani wapo vitani na wanakufa kwa ajili ya watu wa Urusi.
Aidha, baadaye alichapisha video yake akiwa katika makao makuu ya kijeshi, ambayo yanasimamia mapigano nchini Ukraine, na kudai kuwa majeshi yake yamechukua udhibiti wa vituo vya kijeshi katika mji huo, ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege.
Video na picha zilizochapishwa mtandaoni, zikiwemo na shirika la habari la TASS la Urusi, zilionyesha watu wenye silaha wakizunguka majengo ya utawala huko Rostov na vifaru vilivyowekwa katikati mwa jiji ingawa haikufahamika watu hao wenye silaha walikuwa ni akina nani.
Ili kuzuia vitendo vya kigaidi vinavyowezekana katika eneo la jiji la Moscow na mkoa wa Moscow, operesheni imeanzishwa na tayari kamati ya kitaifa ya mapambano ilinukuliwa na mashirika ya Kirusi ikisema Wagner wamedanganywa na kuingizwa kwenye tukio la uhalifu.