Walimu wa shule za msingi na sekondari nchini Kenya wametakiwa kuripoti katika shule wanazofundishia kuanzia Septemba 28, Jumatatu ili kujiandaa na kufunguliwa kwa shule nchini humo.
Kwa mujibu wa mtandao wa Citizen umeandika Waziri wa elimu George Magoha, amesema siku rasmi ya kufunguliwa shule itatangazwa baada ya kamati kufanya mazugumzo.
“Si mimi ninayetoa tarehe ya kufungua shule, nitakaa meza moja na kamati na kujadili siku ya kufungua shule” amesema Prof. Magoha.
Naye mwenyekiti wa tume ya elimu, Sara Ruto kutoka Taasisi ya maendeleo ya mitaala Kenya (KICD), amependekeza shule kufunguliwa katikati ya mwezi Oktoba.
Aidha, wanafunzi ambao wanafanya mitihani ya mwisho watawasili shuleni kwanza na wanafunzi wengine watarejea shule ndani ya wiki chache.
Madarasa yanayotarajiwa kurudi shuleni ni darasa la saba, darasa la nane, kidato cha tatu pamoja na nne.