Serikali ya Rwanda imetangaza kulegeza masharti ya amri za kuwazuia watu majumbani ili kupambana na maambukizi ya virusi vipya vya corona.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais Paul Kagame, Aprili 29, 2020 uamuzi wa kulegeza masharti hayo utaanza kufanyiwa kazi rasmi kuanzia Mei 4, 2020.

Sehemu ya uamuzi wa kikao hicho ni pamoja na kufungua shule mwezi Septemba mwaka huu, huku sehemu za starehe na nyumba za ibada zikiendelea kufungwa.

Taarifa ya kikao hicho imemkariri Waziri Mkuu, Edouard Ngirete imeeleza kuwa kuanzia wiki ijayo, biashara za umma na binafsi zitafunguliwa, lakini wafanyakazi muhimu pekee ndio watakaoruhusiwa kwenda katika sehemu za kazi. Pia, usafiri wa umma utaruhusiwa kwa masharti maalum.

“Usafiri wa umma utaanza kufanya kazi jijini Kigali lakini wamiliki wa vyombo hivyo watapaswa kuhakikisha kuwa abiria wanakaa kwa nafasi na waliovaa barakoa ndio watakaoruhusiwa kupanda,” alisema Waziri Mkuu wa Rwanda.

Hata hivyo, usafiri wa umma na binafsi umeruhusiwa katika jiji la Kigali pekee, hii ikimaanisha kuwa usafiri wa aina hizo hautaruhusiwa kuvuka mipaka ya jiji hilo hadi itakavyoamliwa vinginevyo.

Waliopewa nafasi ya kuingia na kutoka ndani ya jiji hilo ni wale tu wanaosafirisha bidhaa na huduma muhimu kama madawa, vyakula au wanaosafirisha wagonjwa kwa ajili ya matibabu.

Hadi sasa Rwanda ina jumla ya visa 243 vya corona, hii ni baada ya visa vipya 18 kutangazwa saa chache kabla ya uamuzi huo. Waziri wa Afya alisema kuwa wengi waliobainika kati ya hao 18 ni madereva wa magari ya mizigo kutoka nchi jirani za Afrika Mashariki.

Rais Kagame amewataka wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya virusi hivyo kwakuwa mapambano bado hayaisha.

Video: Hotuba ya mbowe yatikisa, Mei Mosi chungu kwa wafanyakazi

JPM atoa wito kwa waajiri siku ya wafanyakazi

Waziri aendesha kikao na mtoto mgongoni
Corona: Mbowe wa Chadema kutohudhuria vikao vya Bunge