Katika kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani leo, Mei 3, 2020, Umoja wa Ulaya umekosoa vizuizi vilivyowekewa vyombo vya habari na baadhi ya nchi, wakati huu wa janga la virusi vya corona.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Josep Borrell katika taarifa kwa niaba ya wanachama 27 wa Umoja huo amesema wana wasiwasi kwamba ugonjwa wa COVID 19 unatumika na mataifa mengine kuvikandamiza vyombo vya habari.
Kulingana na taarifa hiyo iliyotoa jana, siku moja kabla dunia kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari, Borrell amesema ni wakati sasa wa kuweka imani kwa waandishi hasa wakati huu wa migogoro ili kuweza kukabiliana na habari za uwongo.
Imeelezwa kuwa waandishi habari wanakabiliwa na vizuizi wakiwa kazini katika mataifa mengi duniani ikiwemo kufungiwa kwa mitandao, vitisho, kushambuliwa, kukamatwa, kufungwa na hata wengine kupoteza maisha.