Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko ameanza ziara ya kikazi katika jimbo hilo lililoko mkoani Geita na kuwataka Watumishi nchini, kusimamia matumizi sahihi ya fedha za Serikali zinazotegemewa na Watanzania katika kuwaletea maendeleo.
Akizugumza katika Mkutano wa hadhara, Dkt. Biteko amesema chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia kila kilichopangwa kufanyika kinaendelea kufanyika kutokana fedha anazotoa katika miradi ya sekta mbalimbali, u kiwemo ule wa umeme wa Julius Nyerere (MW 2115), ujenzi wa Daraja wa Busisi, ununuzi wa ndege, madarasa, vituo vya afya, na utalii.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesifu juhudi zilizofanywa na Dkt. Biteko wakati akihudumu kama Waziri wa Madini na kueleza kuwa amesaidia kuinua mchango sekta ya madini katika uchumi wa nchi na ameahidi kuwa ataendeleza misingi hiyo mizuri ikiwemo ya kufanya utafiti wa madini katika eneo lote la nchi ili wachimbaji wachimbe madini kwa uhakika na hivyo kuongeza mapato ya nchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela amemshukuru Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii ikiwemo shule, hospitali na umeme katika Mkoa Geita, huku Viongozi wa Mkoa huo wakimsifu Dkt. Biteko kwa uchapaji kazi uliomfanya Rais kumuamini na kumpa nafasi.