Wekundu wa Msimbazi Simba, watacheza mchezo wa kirafiki na Mwadui FC ya Shinyanga Jumatatu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda Zanzibar kuweka kambi ya kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Awali, mchezo huo ilikuwa ufanyike Jumapili, lakini Ofisa Habari wa Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema kwamba umeahirishwa kupisha uzinduzi wa kampeni za vyama vya siasa kuelekea uchaguzi Mkuu.

Mchezo huo unatarajiwa kuwapa fursa wapenzi wa Simba SC kumuona kwa mara nyingine mshambuliaji wao mpya, Kelvin Ndayisenga aliyesajiliwa kutoka Burundi.

Akiichezea kwa mara ya kwanza wiki iliyopita, Ndayisenga alionyesha uwezo wa kuridhisha wa kumiliki mpira, kasi na hata kuwatoka mabeki- siku ambayo alifunga bao moja katika ushindi wa 2-1 dhidi ya URA ya Uganda.

Kubwa zaidi- mchezo huo utazidi kumpa picha halisi ya maendeleo ya kikosi chake, kocha mpya Muingereza Dylan Kerr ambaye hadi sasa ameiongoza timu hiyo kushinda mechi zote nane za kirafiki.

Simba SC ya Kerr imezifunga 2-1 Zanzibar Kombaini, 4-0 Black Sailor, 2-0 Polisi, 3-0 Jang’ombe Boys, 3-2 KMKM zote Zanzibar na 1-0 SC Villa na 2-1 URA zote za Uganda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kaseja Rasmi Mbeya City
JK Anaamini Picha Za Mafuriko Ya Lowassa Zinatengenezwa