Wakati Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara msimu wa 2023-24 ikitarajiwa kuanza kutimua vumbi Disemba 20, mwaka huu, Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Mgosi, amesema Simba imesajili kikosi imara kitakachorudisha ubingwa Msimbazi.
Hivi karibuni, Simba Queens iliwatambulisha wachezaji wapya wanne ambao ni Ainembabazi Joanitah kutoka Ceassia Queens ya Iringa, Raticia Nabbosa (Fountane Gate Princess), Diakiese Isabelle kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Elizabeth Wambui (Kenya).
Kabla ya kuanza msimu mpya, Simba queens itashuka dimbani katika mchezo wa Ngao ya Jamii kuashiria ufunguzi wa ligi kwa kuumana na Yanga Princess, katika mechi itakayopigwa Jumamosi (Desemba 09).
Mgosi amesema Simba Queens imesajili kikosi cha ushindi ambacho kinatarajia kuanza kuhesabu makombe katika mechi ya Ngao ya Jamii.
Mgosi amesema timu inaendelea na mazoezi tayari kwa mchezo na Yanga na maandalizi kwa ujumla ya ligi, hadi sasa kikosi kinazidi kuimarika na wachezaji wanaelewana.
“Tunataka kuanza msimu mpya kwa kishindo kwa kufanya vyema katika mechi ya awali, naamini msimu ujao utakuwa wa mafanikio makubwa kwa Simba Queens,” amesema.
Mshambuliaji wa timu hiyo, Mwanahamisi Omari, amesema wachezaji wote wanafanya mazoezi kwa bidii na kujiandaa kikamilifu kwa msimu ujao wa ligi.
Mwanahamisi amesema hana shaka na viwango vya wenzake na anahidi kushirikiana nao kufanya vizuri kurudisha Ubingwa Msimbazi.
“Tuna deni kwa mashabiki na wapenzi wa timu yetu, msimu uliopita ulikuwa na ushindani mkubwa na ndio maana tulipoteza ubingwa lakini msimu huu ni lazima tufanye makubwa,” amesisitiza Mwanahamisi.
Msimu uliopita, Simba Queens ilipokwa ubingwa na JKT Queens na kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili huku Yanga ikishika nafasi ya tatu.