Mlezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ Simba Queens Fatema Dewji, ameitakiwa kila la Kheri timu hiyo kuelekea Michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika itakayoanza kuunguruma Oktoba 30 mjini Rabat, Morocco.

Simba Queens ilitawazwa kuwa Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati sambamba na kukata tiketi ya kucheza Michuano ya Afrika, Mwezi Agosti kwa kuifunga SHE Corporates kutoka Uganda, ikishinda moja kwa sifuri, katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.

Mlezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ Simba Queens Fatema Dewji

Fatema pia ameipongeza Timu hiyo kwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara na CECAFA kwa kuwapa Wachezaji na Benchi la Ufundi zawadi mbalimbali ikiwemo Medali.

Hafla hiyo iliyofanyika leo Ijumaa (Oktoba 21) jijini Dar es salaam, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ akiteta jambo na Kocha Mkuu wa Simba Queens Charles Ayeikoh Lukula wakati wa Hafla ya kuwapongeza wachezaji na Benchi la Ufundi.

Katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake Simba Queens imepangwa ‘Kundi A’ na wenyeji AS FAR (Morocco), Green Buffaloes (Zambia) na Determine Girls (Liberia).

Simba Queens itaanza Kampeni ya kusaka taji la Afrika Oktoba 30 kwa kucheza na wenyeji AS FAR (Morocco), kwenye Uwanja wa Moulay Hassan, mjini Rabat.

Mabingwa Watetezi Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) wamepangwa ‘Kundi B’ sambasamba na timu za Bayelsa Queens (Nigeria), Wadi Degla (Misri) na TP Mazembe (DR Congo).

Wapinzani wataka raia waamue hatma yao
EU wafikia makubaliano bei ya nishati