Imeelezwa kuwa Uongozi wa klabu Bingwa Tanzania Bara Wekundu Wa Msimbazi Simba (Simba SC), umekamilisha mazungumzo ya kumsainisha mkataba mpya nahodha na mshambuliaji wa kikosi chao John Raphael Bocco.
Bocco ni sehemu ya wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, hatua ambayo inaendelea kuzua hofu kwa mashabiki na wanachama wa Simba SC, kuelekea msimu ujao.
Meneja wa mshambuliaji huyo, Jemedari Said Kazumari amesema baada ya kukamilika kwa hatua ya mazungumzo, hatua inayofuata ni kusianiwa kwa kataba mpya baina ya pande hizo mbili.
“Tayari tumekamilisha mazungumzo ya kusainiwa kwa mkataba mpya, hivyo ni uhakika mchezaji wangu ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.”
“Simba SC wamekua waungwana sana katika hili, wameonesha kuthamini mchango mkubwa wa Bocco kwa kipindi chote alichokuwepo klabuni hapo kwa mujibu wa mkataba wake wa sasa, ambao unaelekea ukingoni, ninaamini atapambana na kuisaidia zaidi klabu hii.’ Amesema Jemedari.
Ikumbukwe kuwa Simba SC ilimsajili Bocco mwaka 2017, akitokea Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili uliokuwa na thamani ya Sh milioni 30.