Uongozi wa Simba SC umesema kwa sasa katika hatua ya Robo Fainali hakuna timu nyepesi hivyo timu yeyote ambayo watapangiwa basi watapambana kuhakikisha wanafanya vizuri ili kusonga katika hatua ya Nusu Fainali.
Simba SC tayari wamerejea nchini wakitokea Morroco walipotoka kumaliza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Raja Casabalanca wa Kundi C ambapo licha ya kupoteza mchezo huo tayari walishafuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema wao kwa sasa hawaangalii timu gani ya kukutana nayo wala hawachagui timu ya kukutana nayo na wanachokifanya ni kuhakikisha kuwa wanapambana na timu yoyote watakayopangwa nayo kutokana na ubora wa kila timu zilizopo.
“Kwenye Robo Fainali hatuwezi kusema kuwa eti tunaomba tupangwe na timu fulani hapana, hatuwezi kabisa kusema hivyo kwa kuwa kila timu ambayo ipo katika michuano hiyo ni timu kubwa na inafanya vizuri.”
“Sasa tukianza kuchagua timu ya kukutana nayo tutakuwa sio washindaji wa kweli, yoyote ambaye tutapangwa naye basi tutapambana naye kuhakikisha kuwa tunafanya vizuri na tunaibuka na matokeo ya kutufanya tuweze kusonga mbele zaidii,” amesema Ahmed Ally
Simba SC inasubiri Droo ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika huku ikitarajia kupangwa aidha na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Esperance de Tunis ya Tunisia na Wydad Casablanca ya Morocco.
Simba SC imemaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hivyo kikanuni inapangwa na moja ya timu zilizomaliza nafasi ya kwanza katika Kundi A, B na D.
Droo ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika itafanyika keshokutwa Jumatano (April 05) mjini Cairo nchini Misri.