Kocha Msaidizi wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda ameitangazia vita ya Ubingwa Young Africans, kwa kusema hawatakata tamaa hadi kieleweke.
Simba SC inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ikiachwa kwa tofauti ya alama sita dhidi ya vinara Young Africans yenye alama 53.
Mgunda amesema bado anaona Simba SC ina nafasi ya kutwaa ubingwa msimu huu, japokuwa kuna baadhi ya wadau wa soka wameanza kuitoa kwenye mbio za ubingwa.
Amesema kinachoendelea kwa sasa Simba SC ni kupambana, huku ikiweka malengo ya kushinda michezo yake yote iliyosalia kwa ajili ya kupunguza pengo la alama dhidi ya wapinzani wao.
“Kitu kikubwa kwa sasa tunaendelea kupambana na kuweka malengo ya kuweza kupata matokeo katika michezo yetu ili kuweza kupunguza pengo la alama.”
“Tunataka kuongeza Presha kwa wapinzani wetu, tunajua sio rahisi, lakini kwa kupambana ndani ya uwanjani itawezekana.”
“Tupo kwenye Ligi kwa ajili ya kushindana na ukiangalia Simba SC tumedhihirisha hilo kwa kuendelea kuwa timu pekee inayofukuzana na walio kileleni kwa sasa, kwa kifupi niseme tutapambana hadi kielekewe.” amesema Mgunda
Simba SC itarejea dimbani Ijumaa (Januari 03) kucheza dhidi ya Singida Big Stars itakayokuwa ugenini Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Young Africans ikitarajia kucheza nyumbani dhidi ya Namungo FC Jumamosi (Januari 04).