Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wamejinasibu kuwa tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi dhidi ya Al Merrikh ya Sudan.
Simba SC itakuwa mgeni wa Al Merrikh mjini Khartoum mwishoni mwa juma hili, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuwa na mwanzo mzuri wa hatua ya makundi, kufuatia kuzifunga AS Vita Club na Al Ahly.
Kocha Mkuu wa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa msimu huu 2020/21 DIDIER Gomes Da Rossa amesema, kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo, ambao anaamini utakua mgumu kwa pande zote mbili.
Amesema amewaandaa wachezaji wake kuwa tayari na mpambano huo, huku akiamini Uongozi wa Simba SC utakamilisha taratibu na mipango ya kuhakiksha mambo yanakwenda vizuri kwa wakati wote watakapokua mjini Khartoum, Sudan kwa maandalizi ya mwisho, kabla ya kupambana na wenyeji wao mwishoni mwa juma hili.
“Tayari wapo waliotangulia nchini Sudan kwa ajili ya kuweka mazingira sawa. Ipo wazi kwamba maandalizi ya mpira huwa yanaanza mapema hilo ndilo ambalo linafanyika pia ndani ya Simba.” Amesema Gomez ambaye kabla ya kutangazwa kuwa kocha mkuu wa Simba SC alikua akifanya kazi na Al Merrikh.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Machi 6 utakuwa ni wa tatu kwa Simba ndani ya kundi A ambapo inaongoza msimamo wa ‘KUNDI A’ ikiwa na alama sita.
Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kuanza safari kesho Jumatano (Machi 03) kuelekea nchini Sudan ili kujiweka sawa kwa ajili ya mchezo hu,o huku habari zikieleza kuwa tayari mabingwa hao watetezi wameshawatuma watu wao mapema nchini humo.