Uongozi wa Simba SC umetamba kuwa ulifanya makusudi kuomba mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Sudan Al Hilal ‘Omdurman’, ili kukiandaa vyema kikosi chao, kabla ya kuivaa Horoya AC ya Guinea.
Simba SC ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23, wanatarajia kuanza kibarua chao cha kwanza Jumamosi (Februari 11), ugenini nchini Guinea kwa kuivaa Horoya AC.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema kwa kuzingatia umuhimu wa mchezo huo wa kwanza wa Kundi C, waliona kuna haja ya kujiandaa kupitia mchezo wenye hadhi ya kimataifa, na ndio maana waliialika Al Hilal nchini Tanzania.
“Baada ya kumaliza ratiba ya mchezo wetu wa Ligi Kuu dhidi ya Singida Big Stars na Mchezo wa Kirafiki dhidi ya Al Hilal, kikosi chetu kinaendelea na maandalizi ya kuivaa Horoya AC katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi.”
“Uongozi wetu uliona kuna haja ya kucheza mchezo mmoja wa Kimataifa wa Kirafiki wenye hadhi ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa, tumecheza dhidi ya Al Hilal na Benchi letu la ufundi limeona mazuri na mapungufu ya kikosi chetu.”
“Tunaendelea na maandalizi ya kuikabili Horoya AC kabla ya kuanza safari ya kuwafuata kwao Guinea, ninaamini kwa siku kadhaa kabla ya safari tutakuwa na maandalizi mazuri chini ya Kocha Robertinho na wasaidizi wake.” amesema Ahmed Ally
Baada ya mchezo dhidi ya Horoya AC, Simba SC itacheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi (18 Februari 2023) dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco, kabla ya kusafiri kuelekea Uganda kukabili Vipers SC itakayokuwa nyumbani St. Mary’s Stadium-Kitende mjini Entebbe, 25 Februari 2023.
7 Machi 2023, Simba SC itarejea jijini Dar es salaam Uwanja wa Benjamin Mkapa kukabili Vipers SC, na siku kumi baadae (17–18 Machi 2023) itaikaribisha Horoya AC Uwanjani hapo, kabla ya kumaliza Hatua ya Makundi Ugenini kwa kuikabili Raja Casabanca itakayokuwa nyumbani Morocco kati ya 31 Machi – April Mosi.