Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea tena kesho Jumatano (Desemba 30), kwa mchezo mmoja kuchezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam, kwa kushuhudia Mabingwa watetezi Simba SC wakipapatuana na Ihefu FC kutoka jijini Mbeya.
Simba SC ambayo imetoka kushinda mchezo wa Kombe la Shirikisho juzi Jumapili (Desemba 27) dhidi ya Majimaji FC waliokubali mabao matano kwa sifuri, itashuka dimbani huku ikiwa na lengo la kuendelea kupunguza pengo lililopo kati yake na Young Africans wanaongoza msimamo wa Ligi hiyo kwa kufikisha alama 43.
Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 32, huku Ihefu FC ikiwa kwenye nafais ya kumi na saba ikiwa na alama 13.
Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza uliozikutanisha timu hizo jijini Mbeya, Simba SC iliibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja yaliyofungwa na John Rafael Boccona Mzamiru Yassin huku bao la kufutia machozi kwa Ihefu likifungwa na Omar Mponda.
Ligi hiyo itaendelea tena Alhamisi kwa michezo mingine saba kuchezwa kwenye viwanja tofauti.