Uongozi wa klabu ya Simba umetishia kuwashtaki Young Aficans kwenye mamlaka ya soka dunaini FIFA, kufuatia mpango wao wa kutangaza usajili wa kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chama bila ya kufuata utaratibu.

Simba wametishia kufanya hivyo, baada ya Makamu Mwenyekiti wa Young Afcans Fredrick Mwakalebela kueleza mipango ya kumfuatilia nyota huyo ambaye alidai kuwathibitishia kuwa mkataba wake uliobaki ni chini ya miezi sita.

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesema watapeleka malalamiko TFF na FIFA kwa kitendo cha klabu ya Young Africans kutaka kumsajili kiungo wao Clatous Chama bila ya kufuata utaratibu.

Akihojiwa kwenye chombo kimoja cha habari mapema leo, Manara alidai Chama ana mkataba wa zaidi ya miezi sita na klabu ya Simba hivyo timu yoyote inayotaka kumsajili bila kufuata utaratibu inafanya makosa.

“Tutaiandika barua TFF kuhusu Mwakalebela kuongea na mchezaji wetu mwenye mkataba na kuvunja kanuni za ligi, katika suala hili hatuwezi kukaa kimya,” alisema Manara

Alichosema Mwakalebela alipohojiwa na vyombo vya habari jana Jumatatu: “Mwakalebela alisema wanaamini, Chama amebakiza mkataba wa miezi sita (6) tofauti na klabu ya Simba inavyosema kwamba bado mchezaji huyo anamkataba wa miaka miwili.”

“Wenzetu wameweka dau wamesema wanataka Dola za Marekani 350,000 ili kumpata Chama ingawa tunajua kabisa amemaliza mkataba. Ningependa kusema kwamba, tunafatilia kwa karibu na tumeanza mazungumzo na Chama na ikiwezekana tungependa aweze kuchezea Young Aficans.”

“Kama tutakubaliana vigezo na masharti ambayo ameyatoa yeye basi atakuwa mchezaji wetu. Nisingependa niwahakikishie wapenzi na wanachama wa Young Africans kwamba tayari tumeshasaini mkataba, nitakuwa nawadanganya ila tunamuhitaji na tunamfatilia na tunaendelea kuwa na mazungumzo naye kama tutafikia mwafaka mzuri tutamleta klabuni kwetu.”

“Kwa mujibu wa maelezo yake mkataba wake unaisha ndani ya miezi sita (6) ijayo, Simba wanasema anamkataba wa miaka miwili (2) kwa hiyo inamaanisha alisaini miaka minne (4) kitu ambacho sisi hatukiamini kama ni kweli.”

“Simba kama wanauhakika watueleze kwamba wanamkataba wa miaka miwili (2) lakini sisi tunaruhusiwa kuongea na mchezaji akiwa amebakiza mkataba wa miezi (6) na ndicho ambacho sisi tunafanya. Kama wanauthibitisho tutapeleka posa kwa barua kama inavyotakiwa”

Karia: Hatma ya ligi kuu ipo mikononi mwa serikali
Corona yasitisha ndoa Kanisa Katoliki