Imefahamika kuwa Uongozi wa Simba SC upo katika mvutano na kiungo mkabaji wa St George ya Ethiopia, Gatoch Panom ambaye amekataa dau la Sh 200Mil alilowekewa mezani ili asaini mkataba.
Muethiopia huyo ni kati ya wachezaji waliokuwepo katika rada za kusajiliwa na Simba SC ambayo imepanga kufanya usajili mkubwa na tishio kuelekea msimu ujao 2023/24.
Kiungo huyo anatakiwa kusajiliwa na Simba SC kwa ajili ya kuiboresha safu ya kiungo ambayo hivi sasa inaongozwa Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin.
Taarifa zinaeleza kuwa Simba SC ipo mbioni kujitoa kwenye mbio za kumsajili kiungo huyo mwenye umbo kubwa anayecheza namba sita, endapo mambo yataendelea kuwa magumu kutokana na msimamo uliowekwa Gatoch sambamba na wawakilishi wake.
Mtoa taarifa hizi amesema kuwa wakala wa kiungo huyo ametaja dau la Sh 250Mil ili mteja wake asaini mkataba huo wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo.
Ameongeza kuwa dau hilo limekataliwa na mabosi wa Simba SC, ambao wenyewe wapo tayari kutoa kitita cha Sh 200Mil pekee ambayo ipo tayari mezani.
“Uongozi umefikia maamuzi ya kuachana na Panom ni baada ya wakala wake kutaja dau kubwa zaidi ambalo ni kubwa sisi tumeshindwa kulitoa.
“Sisi tulikuwa tayari kutoa Sh 200Mil, lakini wakala wa mchezaji yeye ametutajia Sh 250Mil ambazo ni nyingi kwa sasa kwetu, kwani tunahitaji kufanya usajili mkubwa wa wachezaji wapya.
“Hivi sasa tupo katika mipango ya kumtafuta kiungo mwingine wa aina yake atakayekuja kuichezea Simba SC katika msimu ujao, amesema mtoa taarifa huyo.