Kikosi cha Simba SC kinatarajia kucheza Michezo miwili ya Kirafiki baada ya kurejea kambini juzi Jumanne (Agosti 29), kujiandaa na mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Raundi wa Pili Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Simba SC itacheza na Mabingwa wa Zambia Power Dynamos Septemba 16 mjini Ndola Zambia, kisha itamalizia nyumbani Jijini Dar es salaam kwa mchezo wa mkondo wa pili ambao utatoa matokeo ya jumla kwa timu itakayotinga hatua ya Makundi.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amezungumza na Waandishi wa Habari leo Alhamis (Agosti 31) jijini Dar es salaam na kusema: “Tumerejea mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo unaofata dhidi ya Power Dynamos. Wachezaji wote wamerejea isipokuwa golikipa Ayoub kutoka Morocco ambaye anarejea leo na moja kwa moja atajiunga na wenzake.”
“Katika kipindi chote cha kambi tunatarajia kucheza michezo miwili ya kirafiki. Tunasubiri uthibitisho wa timu ambazo tutacheza nazo, moja ya nje na nyingine ya ndani. Lengo letu kama Simba ni tupate mechi ngumu, mechi ya kiushindani.”
Katika hatua nyingine Ahmed Ally amesema Uongozi wa Simba SC umeandaa usafiri maalum kwa ajili ya Mashabiki na Wanachama ambao watahitaji kwenda Ndola, Zambia kuishangilia timu yao katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza dhidi ya Power Dynamos.
“Kuelekea mechi yetu dhidi ya Power Dynamos tunategemea kupeleka mashabiki kama ilivyo kawaida yetu tunapokuwa na mechi kwenye nchi za jirani tunatumia basi kupeleka mashabiki. Bahati nzuri Zambia tumeshawahi kwenda huko.
“Tulipokea maoni tutumie treni na tukafanya mazungumzo na wakawa tayari kutupa punguzo maalumu lakini ratiba za safari ya treni zinapishana na mechi yetu. Utaratibu ambao umeandaliwa na Simba ni tutatoa basi hadi Ndola, Zambia na litarejea nchini baada ya mechi.”
“Basi litaondoka nchini kwenda Zambia tarehe 13, Septemba saa 1 usiku na tutafika Ndola, Zambia tarehe 15, Septemba.
“Tarehe 17, Septemba baada ya mechi basi litaanza safari kurudi Tanzania. Kwa yeyote ambaye anataka kuungana nasi afike ofisini.
“Kwa kila mtu gharama ni Tsh. 200,000 na anatakiwa kuwa na pasi ya kusafiria na kadi ya manjano. Mwisho wa kupokea nauli ni tarehe 10, Septemba.” Amesema Ahmed Ally.