Uongozi wa Simba SC umeendelea kutengua fitina zote walizoandaliwa na wapinzani wao Primeiro De Agosto ya Angola kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo sasa wataondoka nchini Angola mara baada tu ya mchezo wao kumalizika.

Kesho Jumamosi (Oktoba 08) Alfajiri, Simba SC wataondoka Dar es salaam kwa ndege ya kukodi tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumapili (Oktoba 9), katika Uwanja wa De November 11, majira ya saa 10:00 kwa saa za Angola, huku ukitarajiwa kurudiwa Oktoba 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Pamoja na uwepo wa usalama katika msafara wa kuelekea Angola, bado Uongozi wa Simba SC wamejadiliana kuona timu inarejea muda mfupi tu baada ya mchezo huo, ili wachezaji wapate muda wa kupumzika na kuanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

“Kuna njama za fitina tumezigundua kwa wapinzani wetu hivyo kuepuka hilo ni bora turudi mara tu baada ya mchezo kumalizika, maana jamaa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanatuvuruga ili tusiweze kusonga mbele, jambo ambalo tayari tumepata taarifa za kina kutoka kwa watu wetu muhimu.”

“Kwenda na ndege pekee hakukufanyi kuondoa fursa kwa wapinzani wako kukufanyia madhara nje ya uwanja, maana ikumbukwe ile ni nchi yao na jamaa wanatokea jeshini, hivyo kama tukisema tuzubae kule baada ya mchezo itatugharimu kulingana na taarifa za siri tulizopata hivyo tutavunja kila nia yao ovu ili kulinda mipango yetu,” zimeeleza taarifa kutoka Simba SC

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally, amethibitisha kuwa: “Ni kweli kwa kuwa tutaondoka na usafiri binafsi ni wazi kabisa kwamba hatutakuwa na muda tena wa kulala kule, japo bado tunaangalia nini kitafaa zaidi.”

Nasredine Nabi: Hata sisi tunawafahamu vizuri
Kenya na Ethiopia zajadili uhusiano wao kiuchumi