Rais wa Kenya, William Ruto amekutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed kujadili ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kimkakati kati ya nchi hizo mbili kuhusu masuala ya kikanda.

Hii inakuwa ni ziara ya kwanza ya Rais Ruto nchini Ethiopia, baada ya kuchaguliwa kuliongoza Taifa la Kenya na ikumbukwe kuwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed alishiriki hafla ya kuapishwa kwa Rais William Ruto jijini Nairobi, Septemba 13, 2022.

Ethiopia na Kenya, ni nchi ambazo zina urafiki na ushirikiano wa muda mrefu unaozingatia manufaa ya pande zote mbili na ziara hiyo pia inakuja huku kukiwa na vita vinavyoendelea kati ya wanajeshi wa Ethiopia na kundi la Tigray la People Liberation Front (TPLF).

Mazungumzo kuhusu mzozo unaoendelea wa Tigray, yanatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika mkutano kati ya viongozi hao wawili ambapo hapo awali, Rais Ruto alikuwa amethibitisha kuwa utawala wake utachukua jukumu kubwa katika kuongoza mazungumzo ya amani kati ya eneo hilo.

Tayari, Umoja wa Afrika AU, umeandaa mazungumzo ya ngazi ya juu nchini Afrika Kusini kuhusu mzozo huo wa muda mrefu, huku Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta akitarajiwa kuwa sehemu ya wasuluhishi.

Simba SC kurudi Dar es salaam Jumapili
Panya auwa watu 37, wamo watoto 24