Kikosi cha Simba SC kinatarajia kuondoka Julai 14 kuelekea mji wa Ismailia-Misri, tayari kwa Kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ pamoja na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho Barani Afrika ‘CAF’.
Simba SC imedhamiria kufanya makubwa msimu ujao, baada ya kuambulia patupu msimu wa 2021/22, kwa kupoteza mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ yaliyokwenda upande wa Young Africans.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema maandalizi ya safari ya kuelekea Misri yanaendelea vizuri, na kikosi kitaondoka Dar es salaam sambamba na Kocha Zoran Maki ambaye ametambulishwa rasmi leo jumanne (Julai 12), katika mkutano na waandishi wa habari.
“Tarehe 14 mwezi huu kikosi chetu kitaondoka Dar es salaam kuelekea Misri, ambako tutaweka Kambi hadi Agosti 05 mwaka huu, tutaondoka na Wachezaji wote, isipokua wale ambao watakua na jukumu la timu ya Taifa,”
“Wachezaji watakaobaki watajiunga na timu watakapomaliza jukumu la timu ya Taifa, tukiwa Misri tunaamini kikosi kitakua na maandalizi mazuri na kitakua na wasaa kabambe wa kutambua mbinu za Kocha wetu mpya.”
“Tukirejea Dar es salaam Agosti 05 tutakuwa na Simba Day na baadae tutakua na mchezo wa Ngao ya Hisani.” Amesema Ahmed Ally Simba SC itaweka Kambi ya kujiandaa na msimu mpya nchini Misri kwa mara ya Kwanza, baada ya kufanya hivyo katika nchi za Afrika Kusini na Morocco kwa misimu iliyopita.