Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imetangaza kifo cha mmoja kati ya watoto pacha waliotenganishwa Julai Mosi katika Hospitali hiyo (MNH).

Taarifa iliyotolewa na Hospitali hiyo leo Julai 12, 2022 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Aminiel Aligaesha imeeleza kuwa hali ya pacha huyo, Neema, ilibadilika ghafla akiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na alifariki dunia wakati akiendelea na matibabu Jumapili Julai 10, 2022 saa 3 asubuhi.

“Akiwa ICU hali yake ilibadilika ghafla, Madaktari walijitahidi kurudisha hali yake bila mafanikio na hatimaye kupoteza maisha, tuendelee kumwombea Rehema ambaye bado yupo ICU ili Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe sana,” alisema Aligaesha.

Upasuaji wa kuwatenganisha Watoto hao Neema na Rehema ulifanyika ndani ya masala 7 kwa mafanikio katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo Jopo la Wataalamu 31 walikamilisha upasuaji huo.

Watoto hao mapacha wawili wenye umri wa miezi tisa walizaliwa wakiwa wameungana sehemu ya kifua na tumbo na kwa upande wa umbo la ndani wameungana ini ila kila Mtoto ana ini lake.

Wakiwa hospitali hapo baada ya kutenganishwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alifika kuwajulia hali na kupongeza juhudi zilizofanywa na uongozi mzima wa hospitali hiyo katika kuwatenganisha.

Tanzania imekuwa nchi ya tatu Barani Afrika kufanya upasuaji wa aina hii baada ya Afrika ya Kusini na Misri.

Simba SC kuweka kambi Ismailia-Misri
Simon Msuva: Siwakatishi tamaa Young Africans