Klabu ya Simba SC na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya M-Bet zimetangaza Thamani ya Udhamini wa Mkabata wa Miaka Mitano walioingia mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Simba SC ilitangaza kuingia Mkataba mpya na Kampuni hiyo, baada ya kumaliza mkataba na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya SportsPesa mwishoni mwa msimu uliopita.
leo Jumatatu (Agosti Mosi) Simba SC na Kampuni hiyo zimeanika wazi thamani ya udhamini huo katika hafla maalum iliyohudhuriwa na Wadau wa Klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na Waandishi wa Habari, jijini Dar es salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Johari Rotana Mkurugenzi wa Masoko wa M-Bet Allen Mushi alisema: “M-Bet ni kampuni namba moja ya michezo ya kubashiriki sasa tunashirikiana na klabu namba moja Tanzania.”
“Tunaamini kama M-Bet tukishirikiana na Simba tutajitangaza ndani na nje ya Tanzania.”
“Mwaka wa kwanza (Bil 4.670), Mwaka wa pili (Bil 4.925), Mwaka wa tatu – (Bil 5.205), Mwaka wa nne (Bil 5.514) na Mwaka wa tano – (Bil 5.853).”
“Jumla ni Bilioni 26, milioni 168 na Tsh. 5,000.”
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzalez alisema: “Leo ni siku kubwa kwa Simba na M-Bet. Swali kubwa ni kwanini M-Bet. Sababu kubwa ni wameweza kukidhi mahitaji yetu.”
“Kwa ukubwa wa Simba ni lazima kujihusisha na kampuni ambayo inaongoza kwenye biashara ambayo wanafanya. Mkiangalia takwimu M-Bet wanaongoza kwa ukubwa Tanzania.”
“Washirika wote wa Simba kwa sasa wamejitoa kwa Simba tu.”
“Hii ni mara ya kwanza mdhamini mkubwa anakuwa na senior team pekee, huko nyuma mdhamini mkuu alikuwa kwa timu zote lakini sasa timu zingine tunaweza kuzitafutia mdhamini wake.”