Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wamejinasibu kuwa tayari kwa mchezo wa kesho wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhdi ya Al Ahly kutoka nchini Misri.
Simba SC ambao tayari wameshajikusanyia alama tatu za michuano hiyo kwa kuifunga AS Vita Club ya DR Congo, watakua wenyeji wa mchezo huo Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam kuanzia mishale ya saa kumi jioni.
Kocha msaidizi wa kikosi cha Simba SC Seleman Matolla amezungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam na kueleza utayari wa kikosi chao kuelekea mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.
Matolla amesema wamejipanga kupata ushindi kwenye uwanja wa nyumbani, licha ya ukweli kuwa mchezo dhidi ya Al Ahly utakua mgumu, kutoka na wapinzani wao kuwa na uzoefu wa kutoka kwenye michuano ya kimataifa.
“Ni mechi ngumu lakini tumejipanga kupata matokeo mazuri nyumbani” – Neno kutoka kwa Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Al Ahly,” amesema Matolla
Kwa upande wa Nahodha na Mshambuliaji wa Simba SC, John Bocco amesema wachezaji wako tayari kupambana na kufuata maelekezo ya Kocha Gomez na msaidizi wake Matolla watakayopata kwenye mazoezi yao ya mwisho yanayofanyika leo jioni.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu, ni timu kubwa Afrika lakini kwa mbinu tutakazoingianazo kesho, naamini tutapata ushindi”, amesema John Bocco huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi na kuwaamini wachezaji wao.
Msimu wa 2018/19 Simba SC iliibanjua Al Ahly bao moja kwa sifuri Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, baada ya kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao matano kwa sifuri mjini Cairo, Misri.