Uongozi wa Simba SC umeweka wazi kuwa matokeo ya mwisho ndiyo yataamua hatma yao ya kutinga Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, licha ya kuongoza kwa bao 1-0.

Simba SC ilipata ushindi huo katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali dhidi ya Mabingwa watetezi Wydad Casablanca Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi (April 22), na keshokutwa Ijumaa (April 28) itacheza mchezo wa Mkondo wa Pili katika Uwanja wa Mohammed V mjini Casablanca nchini Morocco.

Meneja wa Idara ya Habari Simba Ahmed Ally amesema kuwa wana kazi kubwa kupata matokeo dhidi ya Wydad ugenini, lakini wamejiandaa kupambana hadi tone la mwisho ili kufanikisha azma yao ya kwenda Nusu Fainali msimu huu 2022/23.

“Matokeo ya Uwanja wa Mkapa hayana maana kwamba kazi itakuwa imekwisha bali ni mpaka mchezo wa pili ugenini ambao utakuwa na matokeo ya mwisho na kamili kuamua hatma yetu, tumeshajipanga kupambana katika Uwanja wa ugenini, binafsi nina uhakika tunakwenda Nusu Fainali na Ijumaa tutaandika historia mpya katika bara hili.”

“Tuliushangaza ulimwengu ugenini dhidi ya Zamalek na tumeshawahi kupata matokeo kwenye michezo ya ugenini hivyo tunaamini kazi ya ugenini itakuwa kukamilisha safari ambayo tumeianza katika kufukizia malengo ya kutinga hatua ya Nusu Fainali, inawezekana,” amesema Ahmed Ally

Tayari kikosi cha Simba SC kimeshawasili mjini Casablanca na leo Jumatano (April 26), kinatarajiwa kufanya mazoezi yake ya kwanza kikiwa katika mji huo ambao utashuhudia mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali dhidi ya Wydad Casablanca Ijumaa (April 28).

Arteta apaza sauti safari ya Etihad Stadium
Mikoa ijipange udhibiti mambukizi ya Malaria - Majaliwa