Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka mikoa ambayo ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria ianze kusimamia utekelezaji wa afua za ugonjwa huo, ili kupunguza viwango vya maradhi hayo.

Majaliwa ametoa wito huo wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2023, ambapo Kitaifa yamefanyika Jijini Dar es Salaam.

Amesema, lengo la Serikali ni kutokomeza maambuzi ya ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030 na kwamba upatikanaji wa afua za kinga kama vyandarua vyenye dawa na vitendanishi na dawa za malaria utasaidia sana kupungua kwa idadi ya wagonjwa na vifo vitokanavyo na Malaria nchini.

“Takwimu zinaonesha mikoa inayoongoza kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria ni Tabora una asilimia 23, Mtwara asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 na Mkoa wa Mara una asilimia 15,” amesema Majaliwa.

Ameongeza kuwa, “nimeelezwa kuwa mikoa 9 ina kiwango cha maambukizi chini ya asilimia moja nayo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Songwe, Iringa, Dar es salaam na Mwanza. Kwa namna ya pekee kabisa ninaipongeza sana mikoa yote iliyofanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria.”

Aidha amesema, takwimu zilizopo zinaonesha kuendelea kupungua kwa maambukizi ya Malaria mwaka hadi mwaka kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022. “nitoe wito kwa kuendelea kuongeza nguvu katika mapambano ya kutokomeza Malaria”

Simba SC yaanika mipango ya Casablanca-Morocco
Serikali kuendelea utoaji huduma bora za afya - Dkt. Mollel