Baada ya Simba SC kukosa mataji yote msimu huu, uongozi wa klabu hiyo umetangaza kufanya usajili makini na kujiandaa vizuri kwa msimu ujao 2023/24.
Msimu huu 2022/23 Simba SC imeshindwa kuunguruma na kukosa ubingwa katika michuano yote iliyoshiriki ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na kuishia Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema Simba imeanza kutafuta wachezaji wenye viwango bora na kuwasajili tayari kwa msimu ujao.
Ally amesema kamati ya imeanza kufanya mazungumzo usajili na baadhi ya wachezaji wa ndani na nje ambao wana sifa na viwango bora výa kuisaidia timu.
Amesema kwa kuwa timu imebakiza mechi mbili kabla ya ligi kumalizika, mashabiki waendelee kuwa na utulivu wakati uongozi ukijipanga kufanya usajili wa kishindo.
“Maandalizi ya kufanya usajili wetu na mashabiki yameanza watarajie kuiona Simba ikifanya usajili utakaotikisa, wenye tija na utakaozaa matunda msimu ujao, kila kitu kinaenda vizuri,” amesema Ahmed Ally
Wakati huo huo Kiungo wa Simba SC, Clatous Chama amefungiwa kucheza michezo mitatu na kutozwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Ruvu Shooting, Abalkassim Suleiman.
Chama alifanya tukio hilo Mei 12, mwaka huu wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Ruvu Shooting, ambao ulichezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Katika mechi hiyo ambayo Simba SC iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, Chama alionekana katika vipande vya videoakimkanyaga Kassim.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumapili (Mei 21) na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya TPLB, Chama alimkanyaga kwa makusudi Kassim.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa tukio hilo lilitokea wakati hawagombei mpira, jambo lilosababisha mwamuzi ashindwe kuona.
Kamati hiyo ilieleza kuwa adhabu hiyo imezingatia kanuni ya 41:5 (5.2) ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuhusu udhibiti kwa wachezaji.
Kutokana na adhabu hiyo, Chama atakosa michezo miwili iliyobakí msimu huu pamoja na mchezo wa kwanza msimu ujao.
Simba SC ambayo ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 67, imebakiza mchezo dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union na mechi zote zitachezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi, Dar es Salaam.