Benchi la Ufundi la Simba SC limekiri kuifuatilia Wydad Casablanca katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu ya Morocco, na kubaini mazuri na mapungufu yao.

Mipango ya kuifutilia Wydad Casablanca ilianza baada ya Simba SC kutua salama Morocco, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, utakaopigwa kesho Jumamosi (Desemba 09).

Akizungumza kutoka mjini Marrakech-Morocco, Kocha Msaidizi wa Simba SC, Selemani Matola, amesema walipata muda wa mzuri wa kuwashuhudia wapinzani wao wakicheza mechi ya Ligi Kuu Morocco dhidi ya MC Oudja na kushinda mabao 3-1 ambapo Benchi la Ufundi limepata muda wa kuwasoma Waarabu hao.

Matola amesema kupitia mechi hiyo wameifuatilia Wydad kwa karibu na tayari baadhi ya vitu wameshaanza kuvifanyia kazi.

“Haya ni masuala ya kiufundi sitazungumza sana, lakini hata kama hawatacheza kama walivyocheza katika mechi hiyo, lakini kuna asilimia nyingi hawatabadilika sana,” amesema Matola.

Kuhusu mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa kesho Jumamosi (Desemba 09) kwenye Uwanja wa Marrakech, Matola amesema utakuwa mgumu kwa pande zote mbili, lakini kwao wamejipanga kuhakikisha wanatimiza lengo lao la kutopoteza pointi.

“Siyo kama Wydad Casablanca ilipoteza mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa makusudi, hapana, ilitaka kushinda lakini ilipoteza kwa sababu ya uwezo au ilizidiwa mbinu na timu ilizokutana nazo, kwa hiyo hata mechi yetu sisi hawatakuja eti wafungwe tu kirahisi, kwa sababu hii kwao ni kama mechi ya fainali inabidi ipate ushindi ili irejee kwenye njia sahihi ya kwenda Robo Fainali.

“Sisi Simba SC pia tunalitambua hilo na tunajua haitakuwa mechi rahisi, ni ngumu sana, lakini tutaingia uwanjani kupambana na kuondoka na pointi, tutacheza kwa umakini na utulivu,” amesema Matola.

Hata hivyo alisema Simba pia ni klabu kubwa na yenye malengo makubwa, hivyo na watacheza mechi hiyo kwa kuwabana wenyeji ili kushinda au kuvuna pointi moja muhimu na kuweka hai matumaini ya kusonga mbele.

“Pointi ambazo Wydad Casablanca inazihitaji na sisi tunazihitaji, na sisi pia ni kama fainali, ili tuwe katika njia sahihi ya kusonga mbele ni lazima tupate matokeo ambayo si ya kufungwa, tushinde au kutoka sare na hilo ndilo tunalipogania,” Matola ameongeza.

Amesema mabadiliko ya uchezaji katika kikosi chao ni kitu ambacho kinampa matumaini.

Ratiba EPL yamchefua Klopp
Young Africans kujua mbivu na mbichi leo