Uongozi wa Simba SC umesema upo tayari kumuuza Kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama, endapo utapata dili zinalokidhi vigezo vitakavyowekwa mezani.
Kauli hiyo ya Uongozi wa Simba SC imekuja kufuatia Kiungo huyo kuhusishwa na Mpango wa kuwania na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, itakapofika mwishoni mwa msimu huu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzalez amesema, Chama ni Mchezaji ambaye bado ana mkataba, hivyo Klabu yoyote yenye lengo la kumsajili inapaswa kuwasilisha ofa ili kuanza mazungumzo ya kumsajili.
Amesema Simba SC haiwezi kumbania mchezaji yoyote kuondoka ama kukaa meza moja na Klabu itakayoonesha nia ya kutaka kumsajili mchezaji yoyote wa miamba hiyo ya Msimbazi.
“Kama Young Africans wanamtaka Chama basi walete hela tuwauzie sisi kama Simba SC tunafanya biashara hatuangalii nani anamtaka mchezaji tutachotaka ni hela tu,”
“Wachezaji wetu wote wanauzwa ukija na fedha nzuri tunakuuzia bila hata shida yoyote, Simba haiwezi kumzuia mchezaji kama atatakiwa na Klabu nyingine, kwa hiyo milango ipo wazi kwa yote.” amesema Barbara Gonzalez
Chama alilazimika kurejea Simba SC kupitia Dirisha Dogo msimu uliopita, akitokea RS Berakane ya Morocco ambayo ilimsajili mwishoni mwa msimu wa 2020/21.