Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema kikosi chao hakitacheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya Azam FC nchini Misri.

Klabu hizo zenye Maskani yake jijini Dar es salaam, zimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa ya ‘CAF’ msimu wa 2022/23, katika miji tofauti nchini Misri.

Azam FC imeweka kambi katika mji wa El Gouna tangu juma lililopita, huku Simba SC ikiweka kambi mjini Ismailia ikifikisha siku ya 13 leo Alkhamis (Julai 28).

Ahmed Ally amesema kutokana na muda kuwa mchache, kikosi chao hakitapata nafasi ya kucheza dhidi ya Azam FC nchini Misri, hivyo kitaendelea na ratiba yake ya awali ya kucheza michezo mingine ya kirafiki.

“Kwa ratiba ya michezo ya Kirafiki kwa timu yetu, sijaona nafasi hiyo ya kucheza na Azam FC kwa hapa Misri, kwa hiyo tutaendelea na ratiba yetu kama kawaida na baadae tutarudi nyumbani Dar es salaam.” amesema Ahmed Ally

Simba SC jana Jumatano (Julay 27) ilicheza mchezo wa tatu wa kirafiki dhidi ya Haras El Hodoud na kupoteza kwa mabao 2-0, huku Azam FC ikicheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Wadi Degla na kukubali kupoteza kwa bao 1-0.

Wakati huo huo Ahmed Ally amewataka Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuendelea na Subra kuelekea Wiki ya Simba (Simba Week), ambayo itafikia kilele chake Siku ya Simba (Simba Day) Agosti 08.

Ahmed Ally ametumia kurasa zake za mitandao ya Kijamii kuwasilisha ujumbe kwa Mashabiki na Wanachama ambao wana hamu ya kukiona kikosi chao, na shughuli nyingine za kupamba Wiki ya Simba SC.

Ahmed Ameandika: Shauku ni kubwa kutaka kujua mustakabali wa usajili ndani ya klabu yetu
Shauku kubwa kutaka kujua wachezaji wanaondoka ndani ya klabu yetu.

Shauku ni kubwa kutaka kujua jezi mpya zinazinduliwa lini!!!

Mambo yote hayo muhimu yanafanyiwa kazi na yatakamilika ndani ya wakati
Usajili bado unaendelea deal litakalokamilika mchezaji atawekwa hadharani wala msiwe na presha, tupo kwa ajlli ya kuwajuza.

Wanaondoka ndani ya klabu yetu tupo kwenye mazungumzo nao tutakachokubaliana kwa maslahi ya pande zote mbili tutawajulisha.

Jezi mpya tumefikia pazuri kabla ya Simba Day uzinduzi utafanyika.

MOI yakanusha kukata viungo madereva 'bodaboda'
Maagizo ya Waziri Mkuu kwa Ma-RC