Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka wakuu wa mikoa iliyopo mipakani kutekeleza maelekezo ya Rais ya kufanya ufuatiliaji wa watu waliounda vikundi visivyo rasmi vinavyosababisha migogoro katika sekta ya usafirishaji.

Amesema hayo wakati wa ziara ya kawaida ya Kukagua mwenendo na shughuli za usafirishaji katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma Mkoani Songwe.

Amesema kuwa Serikali haitomvumilia mtu yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo vilivyo tofauti na sheria na taratibu za nchi.

“Ukifanya vitendo viovu utajiingiza kwenye migogoro, kuwa makini usijeingia kwenye mgogoro kwa kutumwa tu, tunazo sheria za nchi,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema kuwa iwapo kuna changamoto yoyote katika sekta ya usafiri inayowahusisha madereva na waajiri wao wasisite kuziwasilisha Serikalini.

“Kama zipo shida njooni sisi tutawapokea na kuwasikiliza ili kutatua shida zenu, malori yanayotoka na kuingia nchini yaachwe, tusijihusishe na migogoro ambayo inatatulika,” amesema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza madereva kwa kuamua kuisikiliza Serikali na kurejea kwenye shughuli za usafirishaji kama awali.

“Taifa linakua kiuchumi katika sekta nyingi ikiwemo sekta ya usafirishaji, kuzuia wengine kufanya kazi ya usafirishaji ni uhujumu uchumi, magari haya yanatuletea fedha, kwani yanahudumiwa na wananchi wengi ambao kwa kufanya hivyo wanajipatia fedha na kuendesha maisha yao.” Waziri Mkuu aliongeza.

Simba SC yaitosa Azam FC Misri
Kocha wa viungo Simba SC afunguka Misri