Uongozi wa Klabu ya Simba umetoa ufafanuzi kwa nini katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Jana Jumanne (Julai 12), hakukuwa na Nembo za Wadhamini katika Mabango.
Simba SC iliitisha Mkutano na Waandishi wa Habari kwa lengo la kumtambulisha Kocha Mkuu Zoran Maki, pamoja na kuanika hadharani mipango ya safari ya Kambi yao huko nchini Misri, ambayo itaanza rasmi kesho kutwa Ijumaa (Julai 15).
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema kutokuwepo kwa Nembo za Wadhamini katika mabango kwenye mkutano wa jana Jumanne, hakumaanishi baya lolote, zaidi ya kuheshimu taratibu za mikataba iliyowekwa.
Ahmed amesema Mkataba wa Simba SC na Wadhamini Wakuu SportsPesa ulifikia tamati tangu walipomaliza Ligi Kuu msimu uliopita (2021/22), na kinachoendea sasa ni mazungumzo ya kusaini Mkataba mwingine.
Amesema kama mazungumzo kati yao na SportsPesa yatakwenda vizuri, watasaini mkataba mpya wakati wowote kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘SFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
“Hakukuwa na Nembo ya Mdhamini Mkuu kwenye Mabango, kutokana na ukweli ni kwamba tumemaliza Mkataba na Kampuni ya SportsPesa, uliomalizika baada ya Ligi Kuu kuisha, bado tupo kwenye mazungumzo kama tutaweza kuendelea nao.” Amesema Ahmed Ally
Kitendo cha kutoonekana kwa nembo za Wadhamini Wakuu kwenye Mabango ya Simba SC, kilibua maswali mengi miongoni mwa wadau wa Soka la Bongo, na wengi walihoji mambo mengi kuhusu tukio hilo.