Mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba wanaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana, Michael Sarpong kwa ajili ya msimu ujao.
Sarpong mwenye umri wa miaka 24, ni mchezaji huru baada ya kuvunjiwa mkataba wake na Klabu ya Rayon Sports ya Rwanda kwa madai ya kumsema Rais wa Klabu hiyo kwenye vyombo vya habari kutokana na madai ya mishahara yake.
Wakati Simba SC ikitajwa kwenye mpango wa kumsajili mshambuliaji huyo, watani zao wa jadi Young Africans nao walihusishwa kwenye mkakati wa kumleta Sarpong nchini.
Simba SC wanaripotiwa kuitaka huduma ya Sarpong na sasa wapo katika hatua ya majadiliano na wawikilishi wa mchezaji huyo mwenye miaka 24, ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa ligi ya Rwanda tangu alipojiunga na Rayon akitokea Dream FC ya Ghana mwaka 2018.
Kiwango kikubwa cha Sarpong msimu wa 2018/2019 kiliisaidia Rayon kutwaa ubingwa wa Rwanda Premier League ambapo alifunga magoli 16 na kuibuka mfungaji bora. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Liberty Professionals pia alifunga magoli 6 katika kombe la FA msimu huo. .
Endapo Simba itamsajili Sarpong, basi ataungana na safu kali ya ushambuliaji inayoundwa na Meddie Kagere na nahodha John Raphael Bocco.