Kikosi cha Simba SC kimetimiza dakika 540 kikicheza mechi sita za michuano ya kimataifa msimu huu bila kuonja ushindi, kitu ambacho hakijawahi kutokea kwao, lakini benchi la ufundi la timu hiyo limetuliza mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kwa kuwaambia watulie, kwani mambo mazuri yanakuja.

Kikosi cha Simba SC kililazimishwa suluhu ugenini na Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mechi ya Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ikiwa ni muendelezo wa mdudu wa sare baada ya awali kutoka sare ya 2-2 kisha 1-1 na Power Dynamos ya Zambia mechi za mchujo.

Pia ilitoka sare ya 2-2 kisha 1-1 mbele ya Al Ahly ya Misri katika African Football League na wiki iliyopita ilibanwa tena na ASEC Mimosas ya lvory Coast kwenye mechi ya makundi.

Rekodi zinaonyesha Simba SC haijawahi kucheza mechi mfululizo kwa idadi kama hiyo bila ushindi, lakini kocha mpya, Abdelhak Benchikha amesema sare waliyopata ugenini sio mbaya sana, kwani bado lina nafasi ikizitumia mechi nne ilizonazo kundini.

Mchezo wa juzi Jumamosi (Desemba 02) ulikuwa wa kwanza kwa Benchikha tangu ajiunge na Simba SC akichukua nafasi ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyetimuliwa baada ya kichapo cha 5-1 kutoka kwa Young Africans katika mechi ya Ligi Kuu ya Novemba 5.

BenchĂ­kha amesema, suluhu hiyo haijaathiri mipango yao, kuelekea mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi B, dhidi ya Wydad Casablanca utakaopigwa nchini Morocco Jumamosi (Desemba 09).

“Hatukupata muda wa kutosha kutengeneza timu, lakini tulipambana na kulinda heshima. Tunashukuru tumepata alama moja, sio mbaya. Bado tuna mechi za kufanya vizuri,” amesema.

Twaha Kidiku aingia kambini Morogoro
Simba SC yarejea kambini kuiwinda Wydad