Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba SC Ahmed Ally amethibitisha taarifa za klabu hiyo kusitisha mpango wa kumsajili Kiungo Mshambuliaji kutoka Niger na klabu ya USGN Victorien Adebayor.
Adebayor alitajwa sana kuwa kwenye mipango ya usajili wa Simba SC, kufuatia kipaji chake kuwavutia baadhi ya viongozi, mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, wakati wa Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2021/22.
Ahmed amesema Simba SC imesitisha mpango wa kumsajili kiungo huyo, kufuatia mahitaji yake ya usajili kuwa makubwa, tofauti na matarajio ya klabu hiyo, ambayo msimu huu imeutema ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
“Klabu yetu ya Simba SC imeachana rasmi na dili la kumpata Mshambuliaji wa Kimataifa wa Niger Victorien Adebayor, na hii ni baada ya kushindwana kwenye upande wa dau analotaka yeye” amesema Ahmed Ally
Hata hivyo Adebayor anatajwa kukamilisha dili la kujiunga na Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika RS Berkane, na wakati wowote mwezi ujao atatambulishwa rasmi klabuni hapo.
Simba SC kwa sasa ipo kwenye mpango wa usajili wa kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa, huku ikihusishwa na wachezaji kadhaa wa kimataifa.