Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin amesema amedhamia kukiwezesha kikosi chake kumaliza kinara wa ‘Kundi D’, katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ baada ya kuibamiza RS Berakane bao 1-0 juzi Jumapili (Machi 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na kufikisha alama 07.
Kocha Pablo amesema hatua ya kuamaliza kinara wa Kundi D ni heshima kwa klabu ya Simba SC Barani Afrika, pia timu yake itapata nafasi ya kucheza Robo Fainali ikianzia ugenini na kumalizia nyumbani.
“Malengo yetu kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho msimu huu ni kuhakikisha tunacheza angalau nusu fainali, na katika kufanikisha hilo ni wazi tunapaswa kufanya kazi kubwa katika michezo yetu ya mwisho ili kuhakikisha tunapata matokeo, yatakayotuvusha na kutinga hatua ya Robo Fainali.”
“Tunataka kumaliza kama vinara wa kundi hili, ambapo hiyo itatusaidia kwa kiasi kikubwa kuwa na bahati ya kuanzia ugenini na kumalizia hapa nyumbani.” amesema Kocha huyo kutoka nchini Hispania.
Simba SC itacheza dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast katika mchezo wa Mzunguuko watano wa ‘Kundi D’ Jumapili (Machi 20) nchini Benin.
Mchezo wa Duru la kwanza uliozikutanisha timu hizo Jijini Dar es salaam, Simba SC ilishinda mabao 3-1, hali ambayo inaongeza chachu ya ushindani kwenye mchezo wa Duru la pili unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka Barani Afrika.
Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi D’ ikiwa na alama 07, ikifuatiwa na ASEC Mimosas yenye alama 06 sawa na RS Berkane ya Morocco, huku USGN ya Niger ikiburusha mkia wa Kundi hilo kwa kufikisha alama 04.