Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kimewasili salama mjini Musoma, Mara kikitokea Jijini Mwanza kilipokua kimepumzika kwa muda.
Simba SC ilianza safari ya kuelekea Musoma, Mara leo asubihi baada ya kuwasili jijini Mwanza jana usiku kikitoka jijini Dar es salaam kwa usafiri wa ndege.
Simba SC imeelekea mjini humo kwa ajili ya mchezo wa mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaowakutanisha na Biashara United Mara, kesho Alhamis katika uwanja wa Karume.
Akizungumzia safari yao, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC, Haji Manara amesema kikosi chao kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo dhidi ya Biashara na wamejipanga kwa vita ya kusaka pointi tatu muhimu.
“Kikosi cha mabingwa wa nchi leo asubuhi kimeanza safari kutoka jijini Mwanza kuelekea mkoani Mara kuifuata Biashara United kwa ajilli ya mchezo wetu wa ligi utakaopigwa kesho.
“Tunajua hautakuwa mchezo rahisi lakini tumejipanga kwa vita ya kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu katika mchezo huo, kwani malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo ulio mbele yetu ili kuzidi kuongeza pointi za kuelekea kileleni mwa msimamo wa ligi,” amesema Manara.
Simba SC imewasili mjini Musoma, Mara na nyota wake wote isipokuwa Wachezaji; Ibrahim Ame, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Rally Bwalya, Ally salami, Kennedy Juma pamoja na Meneja wa kikosi, Abbas Ally ambao waliachwa nchini DR Congo.
Simba ipo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 39, walizozikusanya katika michezo 17 waliyocheza mpaka sasa, Huku Biashara United Mara wakiwa kwenye nafasi ya nne kwa kumilik alama 32.