Kocha Mkuu wa Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin, amesema lengo kuu na klabu hiyo ni kutetea taji la ‘ASFC’ msimu huu 2021/22.

Simba SC inashikilia taji la ‘ASFC’ kwa misimu miwili mfululizo na kesho Jumatano (Februari 16) wataendelea kulitetea kwa mara ya tatu, kwa kucheza mchezo wa Hatua ya 16 Bora dhidi ya Ruvu Shooting.

Katika kuhakikisha mpango wa utetezi wa Kombe la ASFC unatimia msimu huu, Kocha Pablo amesema wamejizatiti kushinda mchezo wa kesho dhidi ya Ruvu Shooting, ili kutimiza azma ya Wanasimba.

Amesema amekiandaa vyema kikosi chake kuelekea mchezo huo utakaoanza saa moja jioni, Uwanja wa Benjamin mkapa Jijini Dar es salaam.

“Sisi ndio mabingwa wa michuano hii na malengo yetu ni kuhakikisha tunavuka hatua hii na kwenda Robo Fainali, na hatimaye tutetee Kombe letu.” amesema Kocha Pablo

Simba SC ilitinga hatua ya 16 Bora, baada ya kuibanjua Dar City mabao 6-0, huku Ruvu Shooting wakiivurumisha nje ya michuano hiyo KMC FC kwa changamoto ya mikwaju ya Penati.

TFF yatangaza Makundi Ligi ya Mikoa 2022
RC Makalla apokea mpango kazi wa zoezi la anuani za makazi DSM