Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC umeanza mazungumzo na wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni, huku ukisema hakuna mchezaji ambaye watamuhitaji kubakia klabuni hapo, wakashindwa kutekeleza mahitaji yake.
Kiungo kutoka nchini Zambia, Clatous Chotta Chama na mshambuliaji kutoka Rwanda Meddie Kagere ni wachezaji pekee ambao mikataba yao itafikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Haji Manara amesema tayari uongozi umeshaanza mazungumzo na wachezaji hao, na yako katika hatua nzuri kwa sababu wanataka kuendelea kuwa na kikosi imara kitakachowapeleka kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Niwatoe hofu mashabiki na wanachama wa Simba, hakuna mchezaji atakayeondoka bila klabu kutaka, wachezaji wote ambao tupo kwenye mzungumzo nao tumefikia hatua nzuri na wote watabaki, nisemu wazi Simba tumejipanga kuwalinda nyota wetu,” amesema Manara.
Manara ameongeza kuwa, kwa sasa hakuna mchezaji wa Simba SC ambaye ataondoka klabuni hpo na kutua klabu nyingine hapa nchini kama alikuwa kwenye malengo yao.
“Simba tuna malengo ya kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa, hivyo ni lazima tuwe na kikosi imara na kwa hapa nyumbani mchezaji wetu ataenda timu gani? Labda kama tutake kumwachia,” amesema Manara.