Afisa Habari wa Singida Big Stars, Hussein Massanza, amebainisha kuwa, baada ya kufanya tathmini ya mwenendo wao kwenye mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, amegundua kitakwimu hawakufanya vizuri kwenye mechi zote walizocheza dhidi ya Simba SC na Young Africans.
Massanza amesema: “Kitakwimu hatukufanya vizuri kwenye mechi zote kubwa, namaanisha dhidi ya Simba na Young Africans, ni kama tumepoteza mechi zote kasoro moja tu ambayo tulipata sare ya 1-1 dhidi ya Simba SC katika uwanja wetu wa nyumbani.
“Hivi inatafsiri kuwa kuna ukomavu wa wachezaji wetu na benchi la ufundi, hawa walijua malengo ya timu ni nini na wakaelekeza nguvu kubwa kuyafanikisha.
“Ingekuwa sio ukomavu basi wangekuwa wanaweka nguvu nyingi kuzikamia mechi hizi kubwa na kupata matokeo ya kufurahisha uma, huku wakidharau mechi zengine na kupoteza alama nyingi.
“Kimsingi tulijua tunahitaji kushinda mechi zote, lakini tunahitaji zaidi kufikia malengo yetu kwa kukusanya alama nyingi, hii imetusaidia sana kufanikiwa msimu huu na pengine ndo imetufanya tuonekane kuwa na sifa ya timu kubwa licha ya kuwa ni msimu wetu wa kwanza.”
Singida Big Stars ambayo huu ni msimu wake wa kwanza kushiriki Ligi Kuu Bara, ilipocheza na Young Africans, mechi zote mbili ugenini na nyumbani ilipoteza, huku ikiambulia sare moja na Simba SC na kupoteza moja.
Matokeo ya mechi hizo ni; Young Africans 4-1 Singida Big Stars, Singida Big Stars 0-2 Young Africans, Simba SC 3-1 Singida Big Stars na Singida Big Stars 1-1 Simba SC.