Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba Sports Club wameanza vyema ligi hiyo mara baada ya kuichapa mabao 3-1 Timu ya JKT Tanzania katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Simba walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa mshambuliaji wake na mfungaji bora wa msimu uliopita, Meddie Kagere ambapo aliwanyanyua mashabiki wake dakika ya pili akifunga bao kwa kumalizia pasi ya kiungo mshambuliaji, Mzamiru Yassin.
Aidha, hadi timu zinaenda mapumziko wenyeji walikuwa tayari wameruhusu bao moja kwa bila lililofungwa na Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ya kiufundi, ambapo dakika ya 58 Meddie Kagere alirudi tena kwenye nyavu za JKT Tanzania akiipatia goli la pili timu yake akipokea pasi kutoka kwa Mzamiru Yassin na kuwanyanyua mashabiki wa Simba waliojitokeza kwa wingi uwanjani hapo.
Akichukua nafasi ya Deo Kanda mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Lipuli FC ya Iringa, Miraji Athumani aliiandikia bao la tatu Simba kwa kichwa mara baada ya kupokea pasi kutoka kwa Meddie Kagere.
Akitokea benchi mshambuliaji wa JKT Tanzania, Edward Songo aliipatia timu yake bao la kufutia machozi mnamo dakika ya 87 akiachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Simba, Aish Manula.
Hadi mwamuzi, Heri Sasii akipuliza kipyenga cha mwisho dakika ya 90 Simba wameibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kujinyakulia alama zote tatu.