Wingi wa Mashabiki wa Klabu nguli za Tanzania Simba SC na Young Africans, umeelezwa kuwa ni moja ya sababu iliyopelekea nchi za Afrika Mashariki kuwa wenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limeridhia ombi la nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, ambao waliomba kupitia jina la Pamoja Bid’ na hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa Fainali za AFCON katika historia ya soka la Afrika.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro, amesema Watanzania wanatakiwa kuziunga mkono timu za Taifa kuweza kutoa hamasa ziweze kufanya vizuri .

Amesema hamasa ya Soka kwa klabu za Young Africans na Simba SC imekuwa chachu kubwa na ndiyo maana CAF wameweka mechi ya ufunguzi wa ‘Super League’ kati ya Simba SC dhidi ya Al Ahly ya Misri itakaofanyika Oktoba 20, mwaka huu jijini Dar es Salaam, ikiwemo uenyeji wa AFCON kwa Afrika Mashariki.

“Wajibu wa Serikali na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ tayari tumeileta AFCON 2027, sasa wajibu upo kwa Watanzania kutoa sapoti kwa timu zao,” amesema.

Waziri huyo amesema kuwa wanaendelea kuweka nguvu ya maandalizi ikiwamo ya ujenzi wa viwanja kwa kuhakikisha vinakamilika mapema na kwa wakati.

Katika hatua nyingine Waziri Ndumbaro amewapa wasaa sekta binafsi kuhakikisha wanajipanga kuchangamkia fursa hizo pindi timu zitakapowasili nchini na kutahitaji huduma mbalimbali chakula, malazi na usafiri.

Wakati huo huo ameipongeza timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kwa kuiondosha lvory Coast katika mchezo wa hatua ya kwanza wa kusaka tiketi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (WAFCON), uliochezwa Jumanne kwa kushinda mikwaju ya Penalti 4-2 kufuatia sare ya mabao 2-2.

“Safari bado haijaisha tuna mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Togo na hii ni muhimu tufuzu WAFCON, tunataka baada ya kupata nafasi AFCON 2027,” amebainisha Dk. Ndumbaro.

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia, amesema kuwa matayarisho yameanza kwa kuwasilisha mapendekezo ya timu ambayo kuhakikisha inafanya vizuri.

Tumeanza maandalizi ya AFCON 2024 nchini Ivory Coast, naamini tutafanya Vizuri kutokana na sapoti kutoka kwa serikali yetu chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Pete ya kuzuia HIV kuzinduliwa hivi karibuni
Wengi wajitokeza uchunguzi wa Saratani, Wanawake wapewa neno