Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, George Simbachawene ameyataka mataifa yaliyoendelea kutoleta bidhaa chakavu za kielektroniki kama runinga na friji kwani vimegeuka kuwa janga.
Amesema mataifa yaliyoendelea yanapoona kitu ni kibaya kwao na hakistahili kwa matumizi huleta Afrika na vitu hivyo husababisha madhara ya kimazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Simbachawene ameyasema hayo juzi wakti akifungua maonesho ya 14 ya kitaifa ya siku ya Nishati Jadidifu yaliyofanyika Jijini Dar es salaam yakiwa na kauli mbiu “Nishati Jadidifu kufikia Tanzania ya viwanda 2025”
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jumuiya ya wadau wa nishati Jadidifu Tanzania (Tarea), imeeleza kuwa licha ya wadau kuhamasisha matumizi teknolijia ya nishati jadidifu, zipo changamoto kubwa za kudhibiti taka zitokanazo na bidhaa za kielektroniki zikiwamo runinga na friji.
Simbachawene ameeleza “Zamani ukiona TV imechakaa ulikuwa unapeleka wilayani kwa mjomba au shangazi na huko zikichakaa zaidi na kuisha matumizi hawana kwa kuzipeleka”
Sasa vifaa vya umeme na elektroniki vinapochakaa vinakuwa janga maana ndani kuna viambata vyenye sumu hivyo inasikitisha kuona TV na friji zilizochakaa zinaletwa kwetu tena” amesisitiza Simbachawene.
Aidha ametoa wito kwa taasisi za umma kama majeshi, magereza, hospitali, shule na vyuo kuingia katika matumizi ya teknolojia ya nishati jadidifu maana miti mingi inakatwa na magereza na shule hivyo, uharibifu wa mazingira ni mkubwa.