Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene ameeleza kuwa kuwa na kitambulisho cha Utaifa (NIDA), hakuhalalishi mtu kuwa ni Raia wa Tanzania.
Simbachawene ameeleza hayo leo Mei 4, Bungeni jijini Dodoma ambapo amesema kuwa Uraia wa Tanzania una Sheria yake ya Uraia na una mchakato wake hivyo kitambulisho hicho ni kwa ajili ya kuwatambua tu hutolewa hata kwa Wakimbizi na hata kwa Wahamiaji wakazi.
“Kwa sasa tunadhani pengine tukipata Vitambulisho vya Taifa ndio tumepata Uraia wa Tanzania, Uraia wa Tanzania una Sheria yake ya Uraia na una mchakato wake, kitambulisho hiki ni kuwatambua tu na vitambulisho hivi vinatolewa hata kwa Wakimbizi, vinatolewa hata kwa Wahamiaji wakazi,” amesema Simbachawene.
Simbachawene amesema mtu kupata kitambulisho hicho sio mwarobaini wa kutokuulizwa na iwapo itagundulika kuwa mtu sio raia basi atanyang’anywa kitambulisho hicho.
“Ukipata kitambulisho hiki sio mwarobaini kwamba wewe umeshamaliza sasa hutaulizwa hapana, utaulizwa na utanyang’anywa hicho kitambulisho kama tukigundua wewe sio Raia wa Tanzania” amesema Simbachawene.