Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu amesema kuwa anataka medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya Riadha yatakayofanyika Budapest, Hungary kuanzia Agosti 19 hadi 27, 2023.

Simbu alitwaa medali ya shaba ya Mashindano ya Dunia yaliyofanyika mwaka 2017 jijini London, Uingereza na ni Mtanzania wa pili kutwaa medali katika mashindano hayo, wa kwanza ni Christopher Isegwe aliyetwaa medali ya fedha mwaka 2005 Helisinki, Finland.

Simbu amesema kuwa amepania kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia.

Amesema kuwa anaendelea vizuri na mazoezi ya maandalizi ya mashindano hayo jijini Arusha chini ya kocha wake, Anthony Muingereza akiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

Simbu ndiye mwakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano hayo baada ya mwanariadha mwingine wa kimataifa, Gabriel Geay kuomba kujitoa ili kushiriki mashindano mengine.

Mwanariadha huyo ambaye amekuwa akifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, amesema kuwa kwa sasa amekuwa akifanya mazoezi kwa gharama zake bila msaada wowote kutoka Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

Hata hivyo, msemaji wa RT, Lwiza John amesema kuwa RT tayari imepeleka kwa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) bajeti ya maandalizi ya Simbu na atarejeshewa gharama zote anazotumia kwa ajili ya maandalizi hayo.

Lwiza amemtaka mwanariadha huyo kuendelea vizuri na maandalizi yake bila wasiwasi wowote, kwani kila kitu kitakwenda vizuri na atarudishiwa gharama zake.

Muingereza amesema kuwa wanaendelea vizuri na mazoezi na wana Imani kubwa mwanariadha wake atafanya vizuri katika mashindano hayo makubwa kabisa ya riadha duniani yanayowashirikisha nyota wengi.

Kupanda kwa dola duniani kwapaisha bei ya Mafuta
Kocha Young Africans aahidi ladha mpya Tanga