Siku chache baada ya kutwaa Tuzo ya mwanamichezo bora wa jumla, mwanariadha Alphonce Simbu, amesema ataendelea kulinda kiwango chake na kufanya vyema katika Mashindano ya Kimataifa.
Simbu alishinda tuzo zilizoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), katika sherehe zilizofanyika Ijumaa (Machi 17) katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Simbu amesema tuzo aliyotwaa imemuongezea morari wa kufanya mazoezi, kusikiliza maelekezo ya walimu wake na atahakikisha anafanya vizuri na kuendelea kuweka rekodi nzuri katika mashindano ya kimataifa.
Simbu amesema ili mwanamichezo awe bora siku zote, anapaswa kufanya mazoezi kwa wakati, kusikiliza ushauri kutoka kwa wadau na kuzingatia mbinu anazofundishwa na kocha wake.
“Bado sijatimiza ndoto, nataka kuwa mwanariadha bora kupitia Michezo ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na mashindano mengine ya kimataifa, juhudi pekee ndizo zitakazotimiza malengo niliyojiwekea,”
“Bado sijatimiza ndoto zangu, nataka kuwa mwanariadha bora kupitia Michezo ya Olimpiki, Jumuiya ya Madola na mashindano mengine ya kimataifa”amesema Simbu.
Mwanariadha huyo alisema atashirikiana na wenzake katika kutangaza, kupeperusha bendera ya Taifa na kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini katika michezo watakayoshiriki.
Pamoja na Simbu kupata tuzo ya mwanamichezo bora wanamichezo wengine waliotwaa tuzo na michezo waliofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ni Rehema Selemani (Tenisi), Amina Ally na Juma Sultan (kabbadi), Madina Idd (gofu), Sophia Lattif na Collins Saliboko (kuogelea).
Wengine Fatuma Kibasu na Ivan Selamani (kriketi), Yusuph Changalawe na Kassim Mbundwike (ngumi za ridhaa) Failuna Abdi, Ibrahim Mgender Ibrahim Class’ (ngumi za kulipwa), Clara Luvanga, Khalifa Kiyanga na Aishi Manula (soka), Regina Serikali (netiboli shuleni) na Raphael Sanga (soka shuleni).
Simbu anashikilia rekodi ya kushika nafasi ya pili, kushinda medali ya fedha katika michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika jijini Birmingham, Uingereza Julai mwaka jana, kwa kukimbia kwa saa 2:12:29.
Februari mwaka huu, Simbu alishika nafasi ya tatu katika mashindano ya riadha ya Osaka yaliyofanyika nchini Japan kwa kutumia muda wa saa 2:06:19.