Kiungo Mshambuliaji wa Tanzania Saimon Happygod Msuva amesema Shirikisho la Soka nchini ‘TFF’ lipo pamoja naye, katika mapambano ya kudai haki zake dhidi ya klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco.
Msuva anakabiliwa na changamoto ya kimaslahi na Uongozi wa klabu ya Wydad Casablanca aliyoitumikia tangu mwaka 2020, hali ambayo ilimfanya kurejea nchini hadi mambo yake yatakapokaa sawa.
Kiungo huyo ambaye aliwahi kuitumikia Young Africans kabla ya kutimkia nchini Morocco mwaka 2017, amesema anaamini suala lake la madai ya kimaslahi ambalo lipo FIFA litamalizwa kwa haki.
“TFF ndio kama baba kwa wachezaji, hivyo wapo pamoja na mimi. FIFA pia tulipopeleka mashtaka wapo pamoja na wachezaji wote wakiangalia haki na kulinda vipaji vyao, kikubwa tusubiri kesi inatoka na majibu gani, nikishindwa sijui itakuaje lakini kama nikishinda basi kuna kiasi kikubwa cha pesa nitapata.” amesema Msuva.
Msuva ametajwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kitakachoingia kambini baadae mwezi huu kwa ajili ya kujiandaa michezo miwili ya Kimataifa ya Kirafiki.