Mshambuliaji wa zamani wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, Simon Msuva ametoa tamko juu ya usajili beki na winga wa kushoto Nickson Kibabage aliyetua Jangwani katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya 2023/24.
Kibabage alitambulishwa rasmi Young Africans usiku wa kuamkia jana Ahamis, na aliambatana na kikosi cha klabu hiyo kuelekea Malawi kwa ajili ya mchezo wa kusherehesha Sikukuu ya Uhuru wan chi hiyo dhidi ya Malawi, jana Alhamis (Julai 06).
Msuva ambaye amewahi kucheza timu moja na Kibabage walipokuwa Difaa El Jadida ya Morocco amesema hana wasiwasi na kinda huyo kutua Young Africans na Mashabiki wengi wataujua ubora wake.
Msuva amesema Kibabage ni mchezaji mshindani ambaye amepata fursa kubwa ya kuendeleza makali yake zaidi ya kile alichokifanya akiwa na Singida Big Stars endapo atapewa nafasi ya kuaminiwa ndani ya timu yake mpya.
“Nakumbuka wakati anarudi Tanzania watu walimbeza kama hivi, lakini nilijua atawashangaza, nikawaona tena watu wakishangaa walipomuona akicheza kama winga badala ya beki kisha akafanya tena vizuri hizo ni nafasi mbili ambazo anajua kuzicheza vizuri, hata hapo Young Africans atawashangaza zaidi, muhimu wamuamini na kumpa nafasi,” amesema Msuva.
“Nimecheza Young Africans naijua ingawaje siijui kwa sasa kama ambavyo wakati nacheza pale, ila naamini ubora wa Kibabage kwa juhudi zake watu watashangaa.
Msuva ameongeza kuwa, Kibabage mara baada ya kusajiliwa na klabu hiyo anatakiwa kuongeza juhudi ya kujituma mazoezini mara mbili ya kile alichokuwa anakifanya katika klabu yake iliyopita.
“Young Africans ni timu kubwa, anatakiwa akienda pale atambue kwamba atawakuta wenzake ambao nao ni bora, kitakachomsaidia ni juhudi zake hasa mazoezini, anatakiwa sasa kufanya mazoezi mara mbili zaidi alivyokuwa akifanya Singida.
“Binafsi huwa nafanya naye mazoezi nitakuwa namkumbusha wakati huu na nitakuwa namfuatilia, amekwenda timu ambayo ina presha kidogo, kila mchezo inataka kushinda kwahiyo ajiweke tayari hata mimi presha hiyo ilinikuta nikiwa pale lakini nilizidisha juhudi sikukata tamaa,” amesema Msuva ambaye kwa sasa anacheza Saudi Arabia.